Mh.Stephen Wasira ambaye ni mbunge wa jimbo la Bunda na waziri wa
kilimo, chakula na ushirika akiwahutubia wananchi katika ukumbi wa chuo
cha benki kuu jijini Mwanza, amesema iwapo chama chake kitamteua
kupeperusha bendera katika kinyang’anyiro cha urais na wananchi wakampa
ridhaa ya kuwa rais wa awamu ya tano, atahakikisha utawala wake
unakabiliana na ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, wizi wa mali na
raslimali za umma.
Aidha Mh.Wasira ambaye amewahi kuhudumu katika wizara mbalimbali za
serikali za awamu zote, amesema iwapo atapata ridhaa ya kuongoza
serikali, atahakikisha kilimo cha jembe la mkono kinabakia kuwa historia
kwa kutoa kipaumbele cha juu katika mapinduzi ya kilimo kwa kuzingatia
kuwa asilimia kati ya 70 hadi 75 ya watanzania wanaishi vijijini na
kuendesha maisha yao kutokana na kilimo na uchumi wa vijijini.
Kuhusu ajira kwa vijana, Mh. Wasira amesema kuwa takwimu za wizara
ya kazi na ajira zinaonyesha kuwa karibu vijana milioni moja wanaingia
katika soko la ajira nchini kila mwaka, lakini ni vijana laki mbili tu
ndio wanaoajirwa jambo ambalo amsema uwiano huo unaweza kusaabisha
matatizo ya kijamii na kisiasa kama hautashughulikiwa.





