Monday, 22 June 2015

KCEE ANASWA SOKONI AKINUNUA MAFUTA YA MAWESE

STAA wa 'Limpopo', Kcee akiwa kwenye soko kuukuu akinunua mafuta ya mawese pamoja na matunda.
LAGOS, Nigeria
STAA wa 'Limpopo', Kcee wikiendi iliyopita alituma picha kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa sokoni.
 Kcee siyo mgeni kwa wadau wa muziki wa Bongo, kwani ameshafanya ngoma na Shetta inayoitwa Shikorobo lakini pia amemshirikisha Diamond Platinumz  katika wimbo mpya wa ‘Love Boat’.
 Kcee alituma picha hiyo akionekana akiwa kwenye soko kuukuu akinunua mafuta ya mawese pamoja na matunda huku baadhi ya wauzaji na wanunuzi waliokuwepo eneo hilo wakimshangaa.
Baada ya kupost picha hiyo, mashabiki waliofanikiwa kuiona walimpongeza kwani ni ngumu sana kwa msanii kuonekana akiwa kwenye soko ‘lililochoka’ akinunua vitu.
Share:

DAVINA AMWANGUKIA MUMEWE

Brighton Masalu
Sorry! Staa wa sinema za Kibongo, Halima Yahya ‘Davina’ anadaiwa kumwangukia mumewe, Abdallah Shakoor ili kurejesha uhai wa ndoa yao ‘iliyokwaruzwa na makucha ya shetani’ ikiwa ni njia ya kurudisha heshima na hadhi yake kwenye familia na jamii kwa jumla.
Staa wa sinema za Kibongo Halima Yahya ‘Davina’.
Habari kutoka kwa chanzo makini kilieleza kwamba, mara kadhaa Davina amekuwa akiomba msaada kwa ndugu, jamaa na marafiki wamsaidie kumuombea msamaha kwa mumewe ili waendelee na maisha kama ilivyokuwa awali.
“Davina amekubali yaishe, unajua anampenda sana mumewe, ‘so’ anahaha kwa ndugu ili wamuombee msamaha,” alisema ‘kikulacho’ huyo wa Davina.
Halima Yahya ‘Davina’ akiwa katika pozi.
Baada ya kuudaka ‘ubuyu’ huo, Ijumaa Wikienda lilizungumza na Davina ambapo alikuwa na haya ya kusema: “Hayo ni maisha yangu binafsi, hayamhusu mtu, kwanza nipo kwenye kikao, niache.”
Share:

Majambazi wamuua sista, wapora fedha

Wananchi wakiangalia sehemu ambayo majambazi walimpiga risasi Sista Clencensia Kapuli Ubungo, Riverside, Dar es Salaam jana. Picha na Michael Matemanga 
Dar es Salaam. Majambazi wamemuua kwa risasi Sista wa Kanisa Katoliki Clencensia Kapuli (50) na kupora kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakijajulikana.
Pia, katika tukio hilo lililotokea jana saa nane mchana eneo la Riverside, Ubungo, Dar es Salaam, dereva aliyekuwa akimwendesha Sista kapuli, Patrick Mwarabu alikatwa kidole gumba kwa risasi.
Sista Kapuli wa Shirika la Mtakatifu Maria wa Parokia ya Mwenyeheri Anwarite, Makoka Jijini Dar es Salaam alikuwa mhasibu wa parokia hiyo ambayo inamiliki Shule ya Sekondari Mwenyeheri Anwarite na Chuo cha Ufundi Stadi Makoka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura aliyefika katika Kituo cha Polisi Urafiki kufuatilia tukio hilo alisema Sista Kapuli na sista mwenzake wakiwa katika gari aina ya Toyota Hilux, walikuwa wakitoka Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City kuchukua fedha na walipita Riverside ndipo walipopatwa na mkasa huo.
“Bado hatujajua ni kiasi gani cha fedha kimechukuliwa kwa kuwa Sista Kapuli ndiye alikuwa mhasibu na ndiye aliyekwenda kuchukua fedha hizo, subirini tutakapokwenda benki kuuliza ni kiasi gani cha fedha alichukua na tutawajuza,” alisema Wambura.
Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ukisubiri taratibu za mazishi.
Shuhuda wa tukio hilo, Gadi Kinyamagolo alisema masista hao walikwenda Riverside kununua mchele katika moja ya maduka ya jumla.
“Mara baada ya kumaliza kununua mchele kama kilo 10 hivi walipanda katika gari wakiwa wawili na kabla ya kuondoka zilifika pikipiki mbili zikiwa na watu wanne, zikasimamisha gari hilo huku mmoja akiwa amevalia kininja na mwingine aliyevaa kawaida, wote wakiwa na silaha. Wengine wawili walibaki kwenye pikipiki.
“Kisha nikaona wanapasua kioo cha nyuma ambapo kulikuwa na sista mmoja na mwingine alikuwa mbele, wote wakiwa na mikoba ambayo majambazi hao waliiomba,” alisema Kinyamagoro na kuongeza:
“Walianza kuwaambia tupe mikoba huku majambazi hao mmoja akiwa amesimama upande wa dereva na mwingine upande wa pili wa gari alipokuwa sista aliyeuawa lakini masista wale hawakutoa mikoba hiyo.”
Kinyamagoro alisema: “Baada ya mabishano, sista aliyekuwa nyuma alifungua mlango na kukimbilia katika duka walilonunua mchele na yule aliyekuwa mbele alipofungua mlango akitaka kukimbia alipigwa risasi shingoni na kutokea upande wa pili na kuanguka nje ya gari.
“Baada ya tukio hilo majambazi hayo yalichukua mikoba miwili na kuondoka nayo. Kwa kuwa mimi nilikuwa karibu nililala chini na eneo hili lilikuwa kimya, watu walikimbia na wengine tulilala tukaacha wafanye kazi yao
Share:

Loveness: Natamani niwe mkufunzi wa michezo

Licha ya kuwa ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa shule za Sekondari (Umisseta) ya msimu huu, Loveness Daudi amekuwa akitumika kama mchezaji kiraka wa Kanda ya Ziwa Magharibi katika mchezo wa netiboli
Kinda huyo aliiongoza Kanda hiyo katika mchezo wa mwisho wa makundi wa netiboli dhidi ya Kanda ya Ziwa, japo walipoteza, lakini Loveness alicheza nafasi ngumu ya kuichezesha timu (Centre), licha ya umri mdogo alionao alitoa ushindani wa hali ya juu kwa wapinzani wao.
“Nimekuja kwenye mashindano nikiwa mchezaji wa timu ya mpira wa mikono, kiongozi wetu alinifuata na kunitaka niwe mchezaji wa kati (Centre) katika timu ya netiboli baada ya nusu ya wachezaji wa netiboli wa Kanda yetu kuwa majeruhi.
“Nilikuwa na uelewa wa mchezo huo kwa kiasi fulani hivyo ninashukuru nimefanya vizuri na na nitaendelea kucheza netiboli hata baada ya hapa kwani ni kipaji changu,” anasema Loveness.
Loveness anayelelewa na babu na bibi yake alizaliwa miaka 12 iliyopita mjini Geita na alianza kushiriki michezo kwa mara ya kwanza akiwa darasa la tano.
“Tuliambiwa kama kuna mtu anahitaji kujiunga timu ya shule ajiandikishe na mimi nikajiandikisha na kuanza mazoezi shuleni.
“Nilipofika darasa la sita nilichaguliwa kwenye timu ya Umitashumta taifa mwaka 2013 katika Mpira wa mikono, ambapo timu yetu ilikamata nafasi ya tatu,” anasema.
Anasema kushiriki kwake michezo hiyo kulianza kumfungulia njia na mwaka uliofuata (2014), aliitwa tena katika timu ya Kanda kabla ya msimu huu kuteuliwa tena kwenye Umisseta akiwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Geita.
Anasema michezo hapa nchini imekuwa na changamoto nyingi hali inayomsukuma kusoma kwa bidii huku akitamani siku moja awe mtaalamu wa michezo ili kusaidia wengine.
“Mfano katika shule yetu, hata kocha hatuna, kipindi cha michezo nahodha ambaye ni mwanafunzi mwenzetu ndiye anabeba jukumu la kocha,” anasema Loveness.
Share:

Christian Bella awatamani Fally Ipupa, P Square, Wiz Kid


mwimbaji wa muziki wa dansi, Christian Bella.
Dar es Salaam. Siku tano tangu kutolewa kwa tuzo za Kilimanjaro KTMA, mteuliwa wa tuzo hizo na mwimbaji wa muziki wa dansi, Christian Bella amesema kuwa ndoto yake kwa sasa ni kurekodi muziki kwa kushirikiana na mwanamuziki nyota, Chris Brown.
Bella ambaye alishindwa kufurukuta katika vipengele vyote alivyowania tuzo huku wimbo wake maarufu ‘Nani Kama Mama’ nao ukishindwa kutwaa tuzo kwa mwaka huu, amebainisha kwamba anachokifikiria kwa sasa ni kolabo za kimataifa na siyo za ndani.
Mkali huyo ambaye anasiemama kama ‘solo artist’, akiimbia pia Bendi ya Malaika, alisema kuwa kwa muda mrefu alikuwa na ndoto hizo na sasa anaamini zitatimia kwa kuanza na wanamuziki wa Afrika.
“Nina ndoto za kufanya kazi na wanamuziki wa kimataifa,” alisema.
Bella alibainisha kwamba ameamua kuanza kufanya kazi na wasanii wenye majina makubwa akiwa na imani kwamba yote yatawezekana iwapo atapata meneja mzuri, atakayeweza kupambana na soko la muziki la nje.
“Kikubwa huwezi kukurupuka kama anavyofanya Diamond. Yeye tayari ana uongozi makini, wewe ukifanya hivyo itakuwa unakosea. Siku moja nikipata meneja kama Babu Tale na Fella, nitakuwa mbali, lakini kwa sasa ni ngumu,” alisema Bella na kufafanua:
“Nikiwa na meneja wa aina hiyo itanisaidia mambo mengi. Kama meneja watakuwa na uwezo wa kufanya baadhi ya mambo, ukichanganya na akili yangu na kipaji nilichonacho, nitaitangaza Tanzania kimataifa. Fikra zangu ni kuanza na Fally Ipupa, baadaye Chris Brown. Lazima uanzie chini, upate ujuzi ndipo upande juu.”
Share:

Chadema ni ‘amsha amsha’


Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Chadema, Mabere Marando akikata utepe kuzindua Bendi ya Wanawake na Operesheni Amsha Wanawake Tanzania katika viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Dar es Salaam jana. Bendi hiyo itatumika kuhamasisha katika mikutano ya Ukawa. Picha na Venance Nestory.
Dar/Hai/Hanang’. Chadema imefanya mikutano mikubwa ya kuamsha wapigakura katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Dar es Salaam na Tanga huku mwenyekiti wake, Freeman Mbowe akisema mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete waliotangaza nia ya kugombea urais ‘wanaivua nguo’ Serikali waliyomo kwa kueleza maovu ya ndani.
Alisema mawaziri hao hawana sauti moja, kila mmoja anazungumza lake kuikosoa Serikali kwa kuahidi kufanya mambo mazuri tofauti na yale yanayofanywa na Serikali ya sasa ya Kikwete.
Hadi sasa makada 38 wa CCM wamechukua fomu za kuomba kuwania urais, miongoni mwao wakiwamo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mawaziri 10 na naibu mawaziri wawili.
Katika kutangaza sifa zao baadhi yao wamekuwa wakijigamba watatatua kero za ufisadi, migogoro ya ardhi, kudorora kwa uchumi na kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mbowe alisema Chadema haiwezi kuiga mfumo huo kwa sababu wana utaratibu wao wa kutangaza nia na kuchukua fomu.
Alisema ratiba yao ya kuchukua fomu za urais ilishatolewa na itaanzia Julai 20 hadi Julai 25, mwaka huu.
“Mawaziri wa Kikwete hawana sera, wamesahau kuwa nao ni sehemu ya serikali hiyo iyo wanayoikosoa. Chadema tuna utaratibu wetu wa kutangaza nia na kuchukua fomu, nafasi ziko wazi,” alisema Mbowe.
Alipoulizwa wamefikia wapi kuhusu mgombea atakayewakilisha vyama vinavyounda Ukawa, Mbowe alisema bado wanafanya mashauriano, muda wowote wakimaliza mgombea wa Ukawa atatangazwa.
“Hii ni vita, hatuwezi kumweka wazi mgombea wetu kwa sababu bado ni mapema. Ukawa bado tunafanya consultations (mashauriano), tukimaliza Watanzania watamjua mgombea wa Ukawa,” alifafanua kiongozi huyo.
Mbowe alipuuza madai kuwa Ukawa inavunjika, akisema haiwezi kuvunjika kama watu wanavyodhani hasa baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kuchukua fomu ya kuwania urais ndani ya chama chake.
Alisisitiza kuwa Ukawa haijazuia chama chochote kuchagua mgombea urais kama walivyofanya CUF bali chama chochote kitasimamisha mgombea wake kisha wagombea wote kushindanishwa na kumpata mmoja wa Ukawa.
“Jambo hili tuliliweka wazi tangu awali, kusimamisha mgombea wa chama siyo hatua ya mwisho, ni sehemu ya mchakato wa kumpata mgombea wa Ukawa,” alisema Mbowe.
Share:

Follow Us

Random Posts

BTemplates.com

Powered by Blogger.
The Magazine

Facebook

Total Pageviews

Random Posts

Recent Comments

Recent Posts

Popular Posts

Blog Archive