Thursday, 8 August 2013

Jambazi sugu la ATM lanaswa Dar es Salaam


 Raia wa Bulgaria akiwa chini ya Ulinzi baada ya kupata kichapo kwa kudaiwa kuiba fedha kwenye mashine ya kutolea fedha (ATM) ya BOA tawi la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam jana.

Kama Benki tuliweka mtambo maalumu na mtuhumiwa huyo alionekana kwenye mtambo wetu, hivyo tuliwaagiza walinzi wetu watakapomwona mtu huyo wamkamate haraka sana,”alisema.

Dar es Salaam. Msako wa wezi wa kwenye Mashine za Kutolea Fedha (ATM), umeanza kuzaa matunda baada ya raia wa Bulgaria kukamatwa akiiba kwenye ATM ya Bank of Africa (BOA), Tawi la Afrikana, Kinondoni, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za benki, mtuhumiwa huyo ambaye hakutajwa jina lake alikamatwa baada ya kamera maalumu zilizowekwa kwenye ATM za BOA, kumtambua kuwa ni mwizi sugu wa benki hiyo anayetafutwa.

Mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 12 asubuhi baada ya mtuhumiwa huyo kuwekewa mitambo maalumu ya kumnasa.
Alisema benki hiyo ilipelekewa malalamiko na baadhi ya wateja kwamba wakienda kutoa fedha kwenye ATM wanakuta akaunti zao hazina salio wakati wanaamini zilikuwa na fedha.

Chanzo hicho cha habari kilidai kuwa baada ya kupelekewa malalamiko hayo, waliweka mitambo maalumu ya kuwawezesha walinzi wa maeneo ya ATM za BOA kumbaini mtu atakayetoa fedha kwa njia ya wizi.

“Kama Benki tuliweka mtambo maalumu na mtuhumiwa huyo alionekana kwenye mtambo wetu, hivyo tuliwaagiza walinzi wetu watakapomwona mtu huyo wamkamate haraka sana,”alisema.

Alisema mtuhumiwa huyo alianza mchezo huo kwa muda mrefu ambapo kwa kutumia kadi za ATM zisizojulikana idadi yake, alikuwa anakwenda kwenye ATM mbalimbali za benki hiyo na kutoa fedha hadi Sh10 milioni.

Kuhusu tukio la jana, mmoja wa walinzi wa BOA aliyejitambulisha kwa jina moja la Frenky alisema mtuhumiwa huyo alipofika kwenye ATM hiyo aliingia na kuchukua fedha ambazo alizipeleka kwenye gari lake. Frenky alisema baada ya kupeleka fedha hizo, alirudi kwa mara ya pili ili achukue fedha nyingine ndipo walinzi hao walimkamata na kumfunga pingu.

“Huyu mtuhumiwa mwenye asili ya Kiarabu alifika na gari lake saa 12 asubuhi, aliingia kwenye ATM na kutoa fedha ambazo hazikujulikana ni shilingi ngapi na kuzipeleka kwenye gari lake, baadaye alirejea tena kwa ajili ya kutoa fedha zingine, wakati anaingia ndipo alipokamatwa na mlinzi aliyekuwa analinda hapo,” alisema Frenky.

Kamanda wa Polisi Kinondoni, Camilius Wambura alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea.

“Ni kweli taarifa nimezipata, mtuhumiwa amekamatwa, bado hatujajua ni kiasi gani ambacho ameiba kwa kutumia mtandao, tunaendelea na uchunguzi,” alisema Wambura.

Tukio kama hili lilishawahi kutokea mkoani Mwanza Februari 19 mwaka huu na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa kushirikiana na maofisa ya Benki ya NMB liliwatia mbaroni watu watatu ambao walidaiwa kuiba kiasi cha Sh700 milioni kwa nyakati tofauti.

Share:

FEZA : Ana bendera tatu mkononi

feza kessy

MCHEZO wa kutoana na nani ataibuka mshindi umekuwa wa kikanda zaidi au ukaribu wa mipaka ya nchi, kuanzia jinsi washiriki wanavyopendekezana na hata Afrika inavyopiga kura katika shindano la Big Brother Africa (BBA).

Kwa wiki tatu mfululizo tumeshuhudia mshiriki wa Kenya akipata kura tatu kila wiki nazo ni za Tanzania, Uganda na Kenya yenyewe.

Washiriki wanaowakilisha nchi za Afrika Magharibi wamekuwa wakiwapendekeza washiriki wa Mashariki au Kusini mwa Afrika.

Mshiriki anayeiwakilisha Tanzania na pengine sasa Afrika Mashariki, Feza Kessy, kesho Jumapili ana mtihani mgumu wa kuiinua Afrika Mashariki kwani ili abaki anahitaji kura kutoka nchi zisizopungua tano.

Katika kikaango yupo na mshiriki kutoka Botswana, Oneal na Bimp kutoka Ethiopia. Kutokana na upigaji kura unaoangalia kanda, Feza angejihakikishia kura ya Ethiopia na ya nchi nyingine zisizo na washiriki.

Kura za uhakika ambazo anazo mkononi mpaka sasa ni ya Kenya, Uganda na Tanzania. Kura ya Ethiopia ameikosa kwa kuwa wanaye mshiriki wao katika kitanzi, Bimp.

Nchi kama Ghana ziliwahi kumpigia kura Feza, lakini mchezo umebadilika na kuna malumbano kati ya Elikem ambaye ni mwakilishi kutoka nchi hiyo.

Kura ya Botswana pia ataikosa kwa kuwa ‘shemeji’, Oneal kutoka nchi hiyo naye yupo kwenye kikaango akitegemea huruma za Afrika ili aweze kubakia katika mashindano hayo.


Washiriki wa Afrika Mashariki

Washiriki kutoka Kenya ni Huddah na Uganda ni Denzel, hao walikuwa wa kwanza kuyaaga mashindano hayo katika wiki ya kwanza.

LK4 kutoka Uganda naye alifuatia wiki moja baadaye na kuwaacha Annabel kutoka Kenya, Nando na Feza kutoka Tanzania wakiwakilisha.

Annabel kwa kutumia kura za nchi tatu yaani Kenya, Uganda na Tanzania, alipona katika kikaango mara nne mfululizo kabla ya kutolewa wiki iliyopita.

Share:

Zanzibar mwezi haukuonekana

Imetangazwa rasmi kwamba zanzibar mwezi haukuonekana hivyo kuwataka wananchi kuendelea na kukamilisha hesabu ya siku 30

Taarifa hiyo imetolewa na kamati ya mwezi kupitia zbc imesema sikukuu ya eid al fitri itakuwa siku ya ijumaa.

Kullu aam waantum bikhair

Share:

Young Killer kuipua ‘Mrs Super Star’




MSANII wa muziki wa hip hop nchini, Young Killer, anatarajia kuachia kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Mrs Super Star’ hivi karibuni.

Msanii huyo kwa sasa anatamba na kibao chake cha ‘Dear Gambe’, ambacho ameimba na Belle 9.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Young Killer alisema yupo katika hatua za mwisho za uandaaji wa kibao hicho, ambacho anaamini kitafanya vizuri kutokana na ubora wa mashairi yaliyomo ndani yake.

“Naamini kazi hii itafanya vizuri kutokana na mashairi ya wimbo huo, naomba wapenzi wa kazi zangu wakae mkao wa kula kwa ajili ya kuipokea,” alisema.

Young Killer alisema kwa upande wa video ya ngoma hiyo, wataonekana baadhi ya wasanii ‘Mastaa’ wa kike ambao wanafanya vizuri katika tasnia ya filamu.

Aliwataja wasanii watakaoonekana katika video ya kazi hiyo kuwa ni Elizabeth Michael ‘Lulu’, Irene Uwoya ‘Oprah’, Jacqueline Wolper, Wema Sepetu na mwanamitindo, Jokate Mwogelo.

Share:

Damu ya Ulimboka yaitesa Serikali

dr ulimboka


SIKU moja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kumfutia kesi raia wa Kenya, Joshua Mulundi, ya kuteka na kujaribu kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, Jeshi la Polisi limeanza sarakasi mpya za kutupiana mpira.

Wakati polisi wakikwepa kuwataja wahusika wa tukio hilo, wadau wamedai kuwa vyombo vya dola vinamkumbatia mmoja wa maofisa wa usalama aliyetajwa na Ulimboka kuhusika na utekaji huo.

Itakumbukwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliunda jopo la maaofisa kutoka kanda hiyo na makao makuu kuchunguza tukio hilo na kutamba kuwa halitatokea tena.

Licha ya tambo hizo, hadi sasa jopo hilo halijawahi kutoa hadharani ripoti ya kile walichokibaini hadi tukio jingine kama hilo likajirudia Machi 6, mwaka huu, alipotekwa na kuteswa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini, Absalom Kibanda.

Watuhumiwa wa tukio la Kibanda pia hawajakamatwa pamoja na Kova kuunda jopo la uchunguzi.

Alipotafutwa jana kuzungumzia uamuzi wa DPP kumwachia huru Mulundi kutokana na kutopatikana ushahidi wa kumtia hatiani kutenda kosa hilo, Kova aligoma katakata kutaja kile kilichobainiwa na jopo la kamati yake ya uchunguzi.

Badala yake Kamanda Kova alisema suala hilo lilikwisha kuondoka kwao na kwamba yeyote anayetaka kujua undani wake ni vema akajaribu kuwasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.

Kova alisema masuala yote hayo ikiwamo watuhumiwa kudaiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi hayako kwake.

“Kwanza uliwahi kunisikia hata siku moja nikimuita mtuhumiwa gaidi, sijawahi, mimi kazi yangu ni kukamata wahalifu mbalimbali wakiwamo wa magari kama haya niliyowaonyesha baada ya kuibwa na majambazi wanaotumia silaha,” alisema Kova.

Tanzania Daima lilimtafuta Kamishna Manumba ili kupata undani wa hatua inayofuata baada ya mtuhumiwa pekee kuachiwa, lakini ofisa huyo naye alikuwa na majibu ya kukwepa.

“Hivi baada ya kuachiwa kilitokea nini? Si umeona alikamatwa tena?” alihoji Manumba ingawa alipobanwa kuwa hakukamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka, alisema sheria inasema kuwa mtu yeyote anaposema uongo, moja kwa moja atakuwa ametenda kosa.

Aidha, alipotakiwa kutolea maelezo mtindo uliozuka wa watu kubambikiziwa kesi za ugaidi, kamishna huyo hakutaka kusikiliza, zaidi ya kusema: “Kwa heri,” kisha kukata simu yake.

Wadau wahoji

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wadau hao walionyesha hofu kwamba kwa sasa kuna hatari ya wananchi kubambikizwa kesi za baadhi ya watu serikalini wanaofanya vitendo hivyo bila kuchukuliwa hatua zozote.

Mkurugenzi wa zamani wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya, alieleza kusikitishwa na kitendo cha polisi kutomtia hatiani ofisa wa Ikulu aliyetajwa kwa jina la Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye aliyeratibu tukio hilo la kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka.

“Kesi ya Dk. Ulimboka mbona ipo wazi, mtuhumiwa yupo wazi, alitajwa na aliyeteswa, serikali ndiyo imemlinda. Kwa hali hii tunakuwa na hofu kuwa vyombo vyetu vya usalama vinatesa watu na kuwalinda watesaji,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa sasa ni kama vile kuna vyombo vya ulinzi vya watu wachache. Kwamba, Tanzania sasa si salama, hakuna utawala bora, haki za binadamu hazizingatiwi wala hakuna demokrasia na uhuru wa mawazo.

Hili si jambo la kuchekea, ni suala la kulaaniwa na kuhuzunisha kwa kila Mtanzania. Ni aibu sana tunapokuwa na serikali inayotesa watu wake,” alisema.

Nkya aliongeza kuwa kwa hali hii Rais Jakaya Kikwete afafanue hadharani kwa Watanzania kuhusu tukio hilo, vinginevyo haeleweki vizuri.

Naye Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema uamuzi wa DPP kuwasilisha mahakamani hati ya kutoendelea na mashtaka hayo ni ishara ya wazi kuwa aliona hayana msingi.

Alisema kuwa mashtaka hayo yalifunguliwa kutumia kisingizio cha kesi kuwa mahakamani ili kudhibiti vyombo vya habari visiandike habari za uchunguzi kuhusu kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka.

Mnyika pia alifafanua kuwa ilikuwa ni njia ya kuzuia Bunge lisijadili na kuihoji serikali. “Uamuzi huu wa DPP sasa umefungua mlango kwa vyombo vya habari kuandika na wabunge kujadili, kwani mmoja wa watuhumiwa ni ofisa wa Usalama wa Ikulu,” alisema.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa kwa uamuzi huo, Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda Kova wajitokeze waseme kuwa walilidanganya taifa kwa mwaka mzima, na kwamba sasa wawaeleze Watanzania nani hasa alimteka na kumtesa Dk. Ulimboka.

Share:

Mwakyembe acharuka

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameionya Kamati ya Nne ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri wa Anga nchini (NCASC) kujiondoa kabla hajaifikia iwapo mzigo wowote wa dawa za kulevya kutoka Tanzania utakamatwa nje ya nchi ukitoka nchini kwa njia ya anga.

Dk Mwakyembe alitoa onyo hilo jana Dar es Salaam wakati akizindua rasmi Kamati hiyo yenye wajumbe 11 na kusisitiza kuwa ina wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege unaimarishwa, ili kudhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini.

“Mimi sidhani suala la kukamatwa kwa dawa za kulevya katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ni dogo,” alisema Dk Mwakyembe na kusisitiza kuwa kashfa ya dawa za kulevya kupitishwa katika uwanja huo, inadhalilisha jina la Baba wa Taifa kitaifa na kimataifa.

Alisema kutowajibika kwa mamlaka zinazohusika na ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege, kumesababisha kuendelea kwa ugaidi wa kimataifa na kusikitishwa na udhaifu unaofanywa na mamlaka hizo hali inayoliletea Taifa fedheha kubwa.

“Sidhani kama mamlaka hizo zinahitaji sheria ili ziwe na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu,” alisema Waziri na kusisitiza kuwa umefika wakati kwa viongozi kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa ili kuleta tija na maendeleo nchini.

Alisema amekuwa akisikia mijadala kuhusu kukamatwa kwa dawa za kulevya, lakini hakuna anayechukuliwa hatua za kisheria kuhusu kashfa hiyo na kuongeza kuwa viongozi wanakataa kuheshimu sheria, hali ambayo alisema inadhalilisha na kushusha hadhi ya viwanja vya ndege nchini.

Baada ya kuzindua Kamati hiyo, Dk Mwakyembe alizuia zawadi zilizoandaliwa kutolewa kwa Kamati inayomaliza muda wake ikiongozwa na Mwenyekiti, Jafari Mpili na kukataa pia kupiga nayo picha ya pamoja badala yake akaomba akutane na Kamati mpya, jana saa nane mchana kujadili kwa kina majukumu.

Awali, katika hutoba yake kwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa NCASC ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Fadhili Manongi, alitaja changamoto kadhaa za kiusalama katika sekta ya anga nchini.

Changamoto hizo ni pamoja na kuchelewa kuridhiwa na Bunge mikataba ya kimataifa inayohusu na usalama wa usafiri wa anga kama vile mkataba wa Beijing na Itifaki ya Mwaka 2010.

Nyingine ni kutojua taratibu za kiusalama na maneno ya kukatisha tamaa kwa maofisa usalama wa viwanja hasa kutoka kwa viongozi waandamizi wa Serikali kwa kauli zao na kutoelewa kanuni za usalama kwa wadau wengi.

Moja ya malengo ya NCASC ni kushauri TCAA hatua za usalama zinazotakiwa katika viwanja vya ndege ili kudhibiti vitisho na ugaidi dhidi ya usafiri wa anga, viwanja na miundombinu yake.

Doa kwa Taifa Juzi katika taraifa yake, Serikali ilisema biashara ya kusafirisha dawa za kulevya imeanza kutia doa taswira ya Watanzania kimataifa. Ilisema uthibitisho ni kwamba katika baadhi ya nchi, kila Mtanzania anayeingia, hivi sasa anachukuliwa kama mshukiwa wa moja kwa moja wa dawa hizo na hivyo kupekuliwa kwa kina.

Serikali ilisema Watanzania waliokamatwa hivi karibuni wakiwa na dawa hizo wamechangia kwa kiwango kikubwa kutoa doa taswira ya nchi. Wiki iliyopita, Mtanzania Jackline Mollel (35), alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Harare, Zimbabwe akidaiwa kuingiza shehena ya dawa za kulevya zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 72.

Kabla ya tukio hilo, Julai, Watanzania wawili, Agnes Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Oliver Tambo, jijini Johannesburg, Afrika Kusini, wakidaiwa kuingiza dawa za kulevya kutoka Tanzania zikiwa na thamani ya mamilioni ya fedha. Walifikishwa mahakamani jijini humo.

Share:

Moto mkubwa wateketeza uwanja wa JKIA

Safari za ndege za ndani ya nchi nchini Kenya zinatarajiwa kurejea kama kawaida baadaye leo baada ya moto mkubwa kuteketeza sehemu ya uwanja rasmi wa kimataifa wa ndege nchini humo JKIA.
Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta ukiteketea

Msemaji wa ikulu ya rais, Manoah Esipisu alisema kuwa ndege za mizigo zitaanza kusafiri lakini akaongeza kuwa serikali haiwezi kusema bayana ni lini safari za kimataifa za ndege zitarejea kama kwaida.


"Tunatarajia kuwa safari za ndege ndani ya nchi zitaweza kurejea kama kawaida baadaye leo, '' alisema Esipisu.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta awali leo ulikua umefungwa baada ya moto mkubwa kutokea katika uwanja huo mjini Nairobi. Moto huo hata hivyo ulidhibitiwa

Hakuna ripoti zozote za majeruhi .

Mwandishi wa BBC katika uwanja huo amesema kuwa kulikuwa na moshi mkubwa uliotoka katika eneo la kuondokea na kuingilia wageni.

Baadhi ya safari za ndege kutoka uwanja huo pia ziliahirishwa wakati zengine zikielekezwa kwenda Mjini Mombasa.

Mwishoni mwa wiki jana baadhi ya wenye maduka ya Duty Free katika uwanja huo walifurushwa baada ya serikali kusema kuwa leseni za wenye maduka zilikuwa zimepitwa na muda.

Huu ni moto mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika uwanja wa Jomo Kenyatta wenye kutumiwa na wasafiri wengi zaidi katika eneo la Afrika mashariki na kati

Uwanja wa ndege wa JKIA ulivyoteketea

Safari za mamia ya wasafiri zimevurugwa na kuachwa nje ya uwanja huo wenye shughuli nyingi zaidi Afrika mashariki
Taarifa za awali zilionyesha kuwa moto huo ulianzia kwenye eneo la uhamiaji katika kitengo cha kupokea wageni kabla ya kusambaa hadi maeneo ya ushuru na mizigo ya abiria.

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana , lakini maafisa wa ngazi ya juu wa serikali wakiongozwa na rais Uhuru Kenyatta walitembelea uwanja huo na kutoa wito uchunguzi ufanyike mara moja. Hata hivyo hawakutoa ishara yoyote ni lini uwanja huo utafunguliwa tena .

Shirika la ndege la kenya -Kenya Airways, ambalo ni kubwa zaidi katika kanda ya Afrika limefuta safari zake zote na kuelekeza ndege zinazoingia nchini katika mji wa Mombasa . Tayari hisa za ndege zimeshuka kwa kiwango cha asilimia 2 . Ndege za kimataifa ambazo zilitakiwa kuondoka leo asubuhi ziliruhusiwa kuondoka bila wasafiri.

Share:

MFANYABIASHARA BILIONEA MOSHI AUWAWA KWA RISASI ISHIRINI

Moshi. Mfanyabiashara tajiri wa Mirerani na Jijini Arusha, Erasto Msuya, ameuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20 kwa kutumia bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), jana mchana.

Erasto anayemiliki vitega uchumi kadhaa na anayeaminika kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wa Mirerani wanaoongoza kwa utajiri,

aliuawa jana saa 7:00 mchana wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

“Eneo la tukio kumeokotwa maganda karibu 21 ya risasi zinazoaminika ni za SMG, yaani mwili ni matobo kila sehemu kwa kweli ameuawa kinyama sana,” alisema polisi mmoja wa Kituo cha Bomang’ombe.

Kufuatia mauaji hayo yaliyotokea kati ya neo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na mji wa Bomang’ombe, mji huo ulifurika magari ya wachimbaji kutoka Moshi, Arusha na Mererani.

Habari za uhakika zilieleza kuwa wauaji wake walikuwa katika pikipiki na baada ya kumminia risasi hizo, walimpora kibegi ambacho haikujulikana kama kilikuwa na madini ama mamilioni ya fedha.

Kulingana na vyanzo vya habari, mfanyabiashara huyo alipigiwa simu na kukubaliana kukutana katikati ya mji wa Bomang’ombe na makutano ya Barabara ya Kia katika Barabara Kuu ya Hai kwenda Arusha.

RPC Kilimanjaro afafanua alivyouawa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema kuwa mfanyabiashara huyo aliuawa saa 7:00 mchana eneo la Mjohoroni kati ya mji wa Bomang’ombe na makutano ya barabara ya Kia.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Eransto alikuwa akitokea Moshi kuelekea Arusha, na alipofika hilo eneo la Mjohoroni alichepuka na kwenda meta 300 nje ya barabara,” alisema.

Kamanda Boaz alisema alipofika eneo hilo, alikutana na vijana wawili waliokuwa na pikipiki ambao waliingia ndani ya gari kwa lengo la kufanya mazungumzo yanayodhaniwa ni ya kibiashara.

Hata hivyo, muda mfupi tu Erasto alishuka kwenye gari lake na kuanza kukimbia na ndipo mmoja kati ya wale vijana alishuka kwenye gari la Erasto na kuanza kumminia risasi nyingi.

Kijana wa Kimasai alivyoshuhudia mauaji

Kijana pekee wa kabila la kimasai anayedaiwa kushuhudia mauaji hayo, aliwaeleza polisi kuwa mara baada ya Erasto kufika eneo hilo la mtaa wa Wasomali, alisimamisha gari na kuwapigia wauaji.

Habari hizo zimedai kuwa vijana wale wawili walipokea simu hiyo na kumtaka ashuke kwenye gari lake la kifahari aina ya Range Rover New Model, ili wafanye biashara ambayo haijui.

Inadaiwa kuwa Erasto alipojaribu kupeleka mkono ili achomoe bastola, mmoja wa wale vijana alianza kumshambulia kwa risasi nyingi ambazo zilimfanya afariki dunia papo hapo.

Kijana huyo wa kimasai anayedaiwa kuwa msaada mkubwa kwa polisi, alidai kuwa baada ya Erasto kudondoka chini, vijana hao walichukua begi alilokuwa nalo na kutokomea.

Pikipiki iliyotumika yapatikana



Taarifa zilizopatikana baadaye jana jioni zilisema pikipiki iliyotumika katika tukio hilo imepatikana katika kijiji cha Olkolili, huko Sanyajuu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.

Kamanda Boaz alithibitisha kupatikana kwa pikipiki hiyo yenye nambari za usajili T316 CLV ikiwa imetelekezwa baada ya gurudumu moja kupata pancha baada ya kufika katika eneo hilo.

“Kwa vile tulikuwa tumesambaza taarifa kila mahali kwamba kuna raia wema walituarifu kuwa kuna watu wametelekeza pikipiki, baada ya kupata pancha na walikuwa wakitembea kwa miguu,” alisema.

Alisema Polisi walikwenda katika eneo hilo na mashuhuda walioshuhudia tukio hilo la mauaji wameitambua pikipiki hiyo kuwa ndiyo iliyokuwa ikitumiwa na wauaji wa mfanyabiashara huyo.

Kamanda Boaz alisema pia kuwa polisi watachunguza kwa kina mawasiliano ya simu ya mfanyabiashara huyo, kwa lengo la kutafuta watu wa mwisho kuwasiliana na marehemu.

Share:

MUME WA PILI WA WASTARA AIBUKA ADAI WASTARA NI MKE WAKE

Na Issa Mnally
MIEZI nane baada ya kufariki dunia mumewe Juma Kilowoko ‘Sajuki’, hatimaye mume wa pili wa staa wa filamu za Kibongo, Wastara Juma aitwaye Ahmed Kushi ameibuka na kudai kwamba anatambua kwamba staa huyo bado ni mkewe na anataka ampatie mwanaye aliyezaa naye.
Kwa muda mrefu kulikuwa na taarifa kuwa Wastara aliachana na mwanaume huyo kwa talaka kabla ya kuolewa na Sajuki lakini kuibuka kwake na madai kuwa bado mwanadada huyo ni mkewe kumezua mshangao mkubwa.



MADAI YA KUSHI
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Kushi alifunguka kwa mara ya kwanza kuwa yeye na Wastara walifunga ndoa ya Kiislamu mwaka 2000 na kujaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume aitwaye Fares.
Alisema: “Kisheria bado ni mke wangu kwa kuwa nilikuwa nimempa talaka moja tu wala hazikufika tatu,” alisema Kushi na kudai kwamba ndoa yake na staa huyo ilidumu kwa mwaka mmoja na nusu na kuvunjika kutokana na kutawaliwa na migororo.
Jamaa huyo alidai kuwa zaidi ya mara tatu amekuwa akimtaka Wastara ampatie mwanaye huyo ambaye kwa sasa ametimiza miaka minane bila ya mafanikio.

KWA NINI WAKATI HUU?
Gazeti hili liliamua kumbana kwa kumuuliza kwa nini ameibuka wakati huu baada ya Sajuki kufa na mbona hakujitokeza kwa zaidi ya kipindi cha miaka kumi iliyopita? Pia akaulizwa kwa nini ameamua kutafuta umaarufu kwa kumdhalilisha? Akaishia kukaa kimya.

WASTARA AFUNGUKA
Baada ya Kushi kuibuka na ishu hiyo yenye utata, gazeti hili lilizungumza na Wastara ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Kuhusu mtoto, kama kweli alikuwa na lengo la kumchukua mwanaye na ananijua, basi atakuwa anawajua wazazi wangu hivyo angefuata utaratibu.
“Hakuna utaratibu kama huo kama kweli anamhitaji mwanaye angeenda kwa wazazi wangu, huko ni kunidhalilisha kwa kuwa ananiona mnyonge baada ya kufiwa na mume wangu Sajuki.
“Kama siyo kunidhalilisha ni nini? Naomba asitumie jina langu kutafuta umaarufu kwa kunichafua. Naomba aache kwa sababu ananiongezea maumivu juu ya maumivu.”
Kuhusu madai kwamba bado ni mkewe, Wastara alilia: “Hivi huyo mtu alikuwa wapi muda wote nikiwa na Sajuki? Mbona hakuibuka wakati mume wangu akiwa hai? Najua anatumia kigezo cha kuondoka Sajuki kunionea lakini Mungu anajua.”

NI KWELI ALIFUNGA NDOA NA KUSHI?
Pamoja na kumbembeleza aeleze kama kweli aliwahi kufunga ndoa na Kushi, Wastara alisema: “Sitaki kumzungumzia mtu, naomba watu wawe na huruma kwangu, wasitumie kigezo cha kumpoteza Sajuki kunidhalilisha.”

SHEHE AMPINGA KUSHI
Gazeti hili halikuishia hapo, lilimtafuta shehe wa Msikiti wa Nuur wa Magomeni-Mapipa jijini Dar, Juma Simba ili kupata ufafanuzi juu ya talaka moja ambapo alimpinga Kushi kwa kusema kuwa kisheria Wastara si mkewe tena.
“Kumpa talaka moja si sababu ya kuendelea kuwa mke wake mpaka leo hii, sheria inasema kuwa Kushi alitakiwa kumrejea Wastara kabla ya miezi mitatu kupita tangu alipompa talaka moja,” alisema na kusisitiza kuwa ndoa hiyo ilishakufa.

YATOKANAYO
Awali ilidaiwa kuwa Wastara aliwahi kuolewa mara mbili kabla ya kufunga ndoa na staa mwenzake wa filamu, Sajuki.
Ndoa ya kwanza ya Wastara aliifunga mwaka 1998 na Juma Mpemba ambaye alibahatika kupata naye mtoto mmoja wa kiume aitwaye Samir.
Sajuki alikuwa mume wa tatu kwa Wastara ambaye naye alibahatika kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Farheen.

Share:

Follow Us

Random Posts

BTemplates.com

Powered by Blogger.
The Magazine

Facebook

Total Pageviews

Random Posts

Recent Comments

Recent Posts

Popular Posts

Blog Archive