Sunday, 11 August 2013

Ronaldo : Kwake ni mwendo wa pesa, starehe na kubadili warembo

KWA sasa anaonekana zaidi kwenye fukwe na kumbi za starehe akiponda raha na mabinti warembo. Hana sababu inayomkwamisha kufanya hivyo, pesa anayo.

Alikitumia vizuri kipindi chake alichokuwa mchezaji, sasa acha atumie pesa yake. Huyu ni Ronaldo de Lima, straika wa zamani wa Brazil aliyetundika daruga Februari 14, 2011.

Soka limempa vitu vingi ikiwa pamoja na utajiri, staa huyo wa zamani wa Barcelona, anatajwa kuwa na pato linalofikia Dola 150 milioni.

Ronaldo aliyezaliwa Septemba 22, 1976 jina lake halisi ni Ronaldo Luis Nazario de Lima. Pesa anayoimiliki kwa sasa ameipata kupitia kazi yake ya kucheza soka. Alipokuwa akitumika uwanjani, aliifanya kazi hiyo kwa ubora mkubwa na kumpatia mikataba minono katika klabu alizopita na mikataba ya matangazo ya biashara.

Kwenye soka, kama kuna watu unaoweza kusema walizaliwa kwa ajili ya kazi hiyo, basi hutakosa kulitaja jina la Ronaldo. Mpira ulizoea miguu yake na ulifanya kile alichokitaka, alipokuwa akiuelekeza kwenda kwenye nyavu.

Kutengeneza pesa

Maisha ya Ronaldo kwenye soka yamedumu kwa miaka 18, akianzia kwenye klabu ya Cruzeiro mwaka 1993 na kuhitimisha soka lake Corinthians mwaka 2011.

Hapo katikati amepita katika klabu za PSV Eindhoven, FC Barcelona, Inter Milan, Real Madrid na AC Milan. Kucheza kwenye klabu hizo kumemfanya atengeneze pesa nyingi kutokana na mishahara yake minono huku akinasa mkataba mbalimbali ya udhamini, ikiwamo kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike. Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Ronaldo katika enzi zake akiwa bado mchezaji, aliingiza pato kati ya Dola 200 milioni na Dola 250 milioni.

Kwa kuwa mara zote Ronaldo alipohama kutoka timu moja kwenda nyingine, ada yake ya uhamisho ilikuwa kubwa, jambo hilo lina maana hata mishahara yake haikuwa ya kima cha chini.

Alilipwa vizuri. Alipotoka Cruizero, inadaiwa uhamisho wake haukuwa chini ya Dola 5 milioni, kabla ya kuweka rekodi alipotoka PSV kwenda Barcelona ambapo miamba hiyo ya Catalan ililipa Pauni 17 milioni, ilikuwa mwaka 1996.

Mwaka mmoja baadaye, Inter Milan ikapanda dau na kumng’oa Nou Camp kwa Dola 19 milioni.

Baada ya kucheza mechi 99 na kufunga mabao 59 akiwa na jezi ya Nerazzurri, Real Madrid ikaja na Euro 46 milioni mwaka 2002 na kuinasa huduma ya mshambuliaji huyo kabla ya kumuuza AC Milan kwa Euro 8.5 milioni miaka mitano baadaye.


Share:

Neville ataka United isimuuze Rooney


MANCHESTER, ENGLAND

JAMANI acheni! Acheni kabisa. Ndivyo ambavyo beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, ameisihi klabu yake hiyo kuachana na mpango wa kumuuza Wayne Rooney hasa kwenda Chelsea.

Tayari Man United imezitupa chini ofa mbili za Chelsea za kutaka kumchukua Rooney, lakini nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 anataka kuandika maombi ya kuuzwa muda wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kutimiza azma yake ya kuhama Old Trafford.

Hata hivyo, Neville anaamini kwamba kocha David Moyes analazimika kumbakiza Rooney kwa sababu ndiye mchezaji muhimu zaidi katika harakati za kuipatia Man United taji la 21 la ubingwa wa Ligi Kuu England.

Neville anaamini kwamba kama Moyes atamuuza Rooney, basi atalazimika kumnunua mchezaji mwenye kiwango cha juu sana kwa ajili ya kupata mbadala.

“Rooney ni mchezaji muhimu sana. Ni bingwa na ni mtu ambaye anaweza kukupatia ubingwa.

Manchester United haipaswi kumuuza kwenda Chelsea, labda kama wakimnunua mchezaji kama Gareth Bale au Cristiano Ronaldo,” alisema Neville.

“Ukiwa na Rooney ujue una dhahabu, mtu ambaye amethibitisha uwezo wake kwa miaka sita, saba, hadi minane iliyopita. Mtu ambaye kila msimu anaonyesha mambo makubwa.

Ana mabao mengi na pasi nyingi za mabao kwa kila msimu. Hata katika msimu uliopita alikuwa hivyo hivyo ingawa hakuwa katika msimu mzuri.

“Atakupa kila unachotaka na hawezi kushusha kiwango chake katika mazoezi. Umuhimu wa Rooney ni mkubwa.

Ni mtu ambaye katikati ya Oktoba wakati uko pointi nne nyuma na inabidi uende kucheza na Chelsea kisha Arsenal, atakaa mbele ya viungo wake wawili na kufanya kila anachoweza, akipigwa viatu lakini huku akiandaa mabao na kufunga.

“Msiidharau thamani ya Rooney kwa mafanikio ya Manchester United katika kipindi cha miaka minane iliyopita na jinsi ambavyo anapendwa na wachezaji wenzake.


Share:

King Kapita aachia Kasema Poa




MSANII wa muziki wa kizazi kipya, King Kapita, ameachia ngoma mpya inayokwenda kwa jina la ‘Kasema Poa’.

Kwa mujibu wa King Kapita, kazi hiyo imeandaliwa katika studio mbili kubwa nchini Nigeria na Tanzania, hivyo anaamini itawashika vilivyo mashabiki kutokana na ubora wake.

King Kapita alisema katika ngoma hiyo amewashirikisha pia Wanigeria, DJ maarufu aitwaye Kalito na DJ Ryder.

King Kapita katika moja ya mashairi ya ngona hiyo anasema: “Sasa tunaimba na kucheza wote, kamwambieni yule mtoto mzuri kasema poa, yanii she say yeahhhh...”

Ngoma nyingine zinazobamba za msanii huyo mmoja wa waasisi wa kundi la Wakacha, ingawa sasa anajitegemea ‘Solo artist’ ni pamoja na ‘Shikamoo Pesa’, ‘Kuna tatizo Kwani’ na sasa kaachia ‘Kasema Poa’.

Msanii huyo aliongeza kuwa, hivi sasa ngoma hiyo inapatikana mtandaoni na kuomba sapoti kutoka kwa wadau mbalimbali wa sanaa.

Share:

Serikali yamgeuka Ulimboka


SIKU chache baada ya Mahakama ya Kisutu kumwachia mtu aliyedaiwa kumteka na kumtesa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, serikali imemshukia daktari huyo na kudai ndiye chanzo cha kukwama kwa dola kukamata watu waliomteka.

Jana Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Eliazer Feleshi, alidai kuwa vyombo vya dola vimeshindwa hadi sasa kuwakamata waliohusika katika shambulio hilo kutokana na Dk. Ulimboka kukwepa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

Feleshi ambaye jana aliambatana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alidai lawama zinazosukumwa kwa Jeshi la Polisi kwa madai ya kushindwa kuwakamata waliomtendea unyama daktari huyo hazina msingi, kwa kuwa mhusika mwenyewe hajafika polisi, licha ya kuitwa mara nyingi kutoa maelezo.

Alisema kama Dk. Ulimboka angetoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kungekuwa na mafanikio makubwa katika kuwasaka na hata kuwatia mbaroni waliohusika katika unyama huo.

“Kila mara mmekuwa mkilaumu polisi wanashindwa kukamata wahalifu lakini tutakamataje kama wenye ushahidi hawataki kutoa ushirikiano?

Kwa mfano mdogo tu ni ‘ishu’ (suala) ya Dk. Ulimboka, hadi leo hajatoa taarifa lakini polisi wanaendelea kusakamwa na kutukanwa tu,” alisema.

Hata hivyo, wakati Feleshi akitoa kauli hiyo, Dk. Ulimboka katika andiko lake alilolitoa mara tu baada ya kurejea nchini kutoka Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu, alimtaja mtu anayeaminika kuwa mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye aliyemteka na kumtesa.

Ulimboka akimtumia Wakili Nyaronyo Kicheere alisema Ighondu na wenzake ni mhusika mkuu katika unyama aliofanyiwa, kauli ambayo imekanushwa mara kadhaa na serikali.

Mapema wiki hii, raia wa Kenya, Joshua Mulundi, aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka aliachiwa na Mahakama ya Kisutu baada ya DPP Feleshi kumfutia shitaka. Hata hivyo Mulundi alikamatwa tena na sasa amefunguliwa mashitaka ya kutoa maelezo ya uongo kwa polisi.

Wakati DPP akisema hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, jana aligoma kuzungumzia shinikizo la kumtaka ajiuzulu kutokana na kukithiri kwa matukio ya raia kumwagiwa tindikali, badala yake amewataka Watanzania kuwa na ushirikiano wa pamoja kukabiliana na uhalifu huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, (IGP) Mwema alishindwa kukubali kujiuzulu wadhifa huo na badala yake alitoa majibu ya jumla huku akiwataka Watanzania kubadilika na kuona suala la kulinda raia na mali zao ni jukumu la kila mmoja na si kazi ya polisi pekee.

Mkuu huyo alisema kuwa Watanzania lazima waelewe kuwa suala la ustawi wa jamii linatokana na uwepo wa amani na utulivu. “Nchi hii si ya mtu mmoja bali ni ya kila Mtanzania, inashangaza kuona asilimia 89 ya Watanzania wanaona suala la kulinda raia ni la polisi, si kweli ni lazima tubadilike,” alisema.

Alisema kuwa jukumu la utu lipo pale pale, hivyo kama taifa wana dhamana ya kuhakikisha suala la matumizi mabaya ya tindikali na dawa za kulevya linakomeshwa.

Mwema alisema kuwa wanalaani vitendo vibaya na vya kikatili vinavyofanywa na mtu mmoja mmoja ambavyo vinaleta hofu kwa jamii.

Alisema kuwa juhudi mbalimbali zinafanywa kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa na hata kumalizwa kabisa. “Tumeamua kuja na mkakati wa pamoja kwa kuwa sasa matukio ya umwagiaji tindikali umeshamiri na hatuwezi kusubiri adhurike mtu mwingine, bali tusaidiane wote kwa pamoja kukomesha haya,” alisema.

Alisema kuwa lengo la kutengenezwa kemikali hiyo haikuwa kutumika vibaya au kumdhuru binadamu, bali ni muhimu kwa ajili ya vyombo vya usafiri na maabara.

“Hata kisu ukiangalia kimetengenezwa kwa ajili ya mambo ya msingi, lakini kikitumika vibaya kinaweza kudhuru watu,” alisema.

Huku akionyesha hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo bila kutaja jina, alisema kuwa ofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mmoja amesimamishwa kazi baada ya kudaiwa kuruhusu kupita kwa mabegi tisa ya dawa za kulevya yaliyokamatwa Afrika Kusini mwezi uliopita.

Mwema alisema kuwa ni muhimu wananchi wakatoa taarifa mapema pindi waonapo mwenendo mbaya wa matumizi ya tindikali hiyo, kwa kuwa ni uhalifu mpya.

“Wananchi ndio waathirika wa kwanza, ni vema wakatoa taarifa mapema ili hatua ziweze kuchukuliwa, maana vyombo vya dola pekee haviwezi kuhimili jambo hilo,” alisema.

Matukio ya kumwagiwa tindikali kwa sasa yameshamiri nchini kufuatia baadhi ya raia kupata ulemavu na wengine vifo, huku Julai 19, mwaka huu mmiliki na mfanyabiashara maarufu wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad, akivamiwa na kumwagiwa maji usoni yanayodhaniwa kuwa ni tindikali.

Ikiwa ni takriban wiki mbili tangu kutokea kwa tukio hilo, juzi wasichana wawili raia wa Uingereza waliofika visiwani Zanzibar kujitolea kufundisha somo la Kiingereza walimwagiwa tindikali majira ya saa 1:15 usiku, Mtaa wa Shangani eneo la mji Mkongwe.

Hata hivyo wasichana hao walisafirishwa jana kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mwaka 2007 Mkurugenzi wa Halihalisi Publishers, Said Kubenea, alimwagiwa tindikali, hatua inayomlazimu kwenda nchini India mara kwa mara kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

Mwaka 2011 wakati wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Igunga, Musa Tesha, alimwagiwa tindikali, huku mkoani Arusha, wilayani Arumeru, Sheikh wa wilaya hiyo, Said Juma Makamba, alijeruhiwa kwa kumwagiwa usoni kimiminika kinachoaminika kuwa tindikali.

Wakati Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, Novemba mwaka jana alimwagiwa tindikali.

Mkemia Mkuu wa Serikali

Katika kikao cha jana, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyere, alipiga marufuku usafirishaji wa tindikali bila kibali na kuagiza wahusika kutunza kumbukumbu kuonyesha ukali wa tindikali na kutoa mrejesho wa kiasi walichouza kuanzia mwezi huu.

Alisema kuwa wasafirishaji wanapaswa kuwa na vibali kisheria ambavyo vimetolewa na ofisi yake.

Profesa Manyere alisema kuwa wauzaji wa rejareja ni lazima wawe wamesajiliwa na wanapaswa kutoa taarifa za mauzo wanayofanya kila baada ya miezi mitatu kuanzia sasa.

Alisema kuwa kuanzia sasa wamiliki wa vyombo vya usafiri hawaruhusiwi kuchukua kemikali hiyo na kwenda nayo nyumbani badala yake wapeleke magari yao. “Wale wa lita moja moja hawaruhusiwi kuuziwa bali itapaswa kuuzwa kuanzia lita tano na kuendelea,” alisema.
Share:

Follow Us

Random Posts

BTemplates.com

Powered by Blogger.
The Magazine

Facebook

Total Pageviews

Random Posts

Recent Comments

Recent Posts

Popular Posts

Blog Archive