Sunday, 11 August 2013

Ronaldo : Kwake ni mwendo wa pesa, starehe na kubadili warembo

KWA sasa anaonekana zaidi kwenye fukwe na kumbi za starehe akiponda raha na mabinti warembo. Hana sababu inayomkwamisha kufanya hivyo, pesa anayo.

Alikitumia vizuri kipindi chake alichokuwa mchezaji, sasa acha atumie pesa yake. Huyu ni Ronaldo de Lima, straika wa zamani wa Brazil aliyetundika daruga Februari 14, 2011.

Soka limempa vitu vingi ikiwa pamoja na utajiri, staa huyo wa zamani wa Barcelona, anatajwa kuwa na pato linalofikia Dola 150 milioni.

Ronaldo aliyezaliwa Septemba 22, 1976 jina lake halisi ni Ronaldo Luis Nazario de Lima. Pesa anayoimiliki kwa sasa ameipata kupitia kazi yake ya kucheza soka. Alipokuwa akitumika uwanjani, aliifanya kazi hiyo kwa ubora mkubwa na kumpatia mikataba minono katika klabu alizopita na mikataba ya matangazo ya biashara.

Kwenye soka, kama kuna watu unaoweza kusema walizaliwa kwa ajili ya kazi hiyo, basi hutakosa kulitaja jina la Ronaldo. Mpira ulizoea miguu yake na ulifanya kile alichokitaka, alipokuwa akiuelekeza kwenda kwenye nyavu.

Kutengeneza pesa

Maisha ya Ronaldo kwenye soka yamedumu kwa miaka 18, akianzia kwenye klabu ya Cruzeiro mwaka 1993 na kuhitimisha soka lake Corinthians mwaka 2011.

Hapo katikati amepita katika klabu za PSV Eindhoven, FC Barcelona, Inter Milan, Real Madrid na AC Milan. Kucheza kwenye klabu hizo kumemfanya atengeneze pesa nyingi kutokana na mishahara yake minono huku akinasa mkataba mbalimbali ya udhamini, ikiwamo kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike. Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Ronaldo katika enzi zake akiwa bado mchezaji, aliingiza pato kati ya Dola 200 milioni na Dola 250 milioni.

Kwa kuwa mara zote Ronaldo alipohama kutoka timu moja kwenda nyingine, ada yake ya uhamisho ilikuwa kubwa, jambo hilo lina maana hata mishahara yake haikuwa ya kima cha chini.

Alilipwa vizuri. Alipotoka Cruizero, inadaiwa uhamisho wake haukuwa chini ya Dola 5 milioni, kabla ya kuweka rekodi alipotoka PSV kwenda Barcelona ambapo miamba hiyo ya Catalan ililipa Pauni 17 milioni, ilikuwa mwaka 1996.

Mwaka mmoja baadaye, Inter Milan ikapanda dau na kumng’oa Nou Camp kwa Dola 19 milioni.

Baada ya kucheza mechi 99 na kufunga mabao 59 akiwa na jezi ya Nerazzurri, Real Madrid ikaja na Euro 46 milioni mwaka 2002 na kuinasa huduma ya mshambuliaji huyo kabla ya kumuuza AC Milan kwa Euro 8.5 milioni miaka mitano baadaye.


Share:

Follow Us

Random Posts

BTemplates.com

Powered by Blogger.
The Magazine

Facebook

Total Pageviews

Random Posts

Recent Comments

Recent Posts

Popular Posts

Blog Archive