Licha ya kuwa ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa shule za Sekondari (Umisseta) ya msimu huu, Loveness Daudi amekuwa akitumika kama mchezaji kiraka wa Kanda ya Ziwa Magharibi katika mchezo wa netiboli
Kinda huyo aliiongoza Kanda hiyo katika mchezo wa mwisho wa makundi wa netiboli dhidi ya Kanda ya Ziwa, japo walipoteza, lakini Loveness alicheza nafasi ngumu ya kuichezesha timu (Centre), licha ya umri mdogo alionao alitoa ushindani wa hali ya juu kwa wapinzani wao.
“Nimekuja kwenye mashindano nikiwa mchezaji wa timu ya mpira wa mikono, kiongozi wetu alinifuata na kunitaka niwe mchezaji wa kati (Centre) katika timu ya netiboli baada ya nusu ya wachezaji wa netiboli wa Kanda yetu kuwa majeruhi.
“Nilikuwa na uelewa wa mchezo huo kwa kiasi fulani hivyo ninashukuru nimefanya vizuri na na nitaendelea kucheza netiboli hata baada ya hapa kwani ni kipaji changu,” anasema Loveness.
Loveness anayelelewa na babu na bibi yake alizaliwa miaka 12 iliyopita mjini Geita na alianza kushiriki michezo kwa mara ya kwanza akiwa darasa la tano.
“Tuliambiwa kama kuna mtu anahitaji kujiunga timu ya shule ajiandikishe na mimi nikajiandikisha na kuanza mazoezi shuleni.
“Nilipofika darasa la sita nilichaguliwa kwenye timu ya Umitashumta taifa mwaka 2013 katika Mpira wa mikono, ambapo timu yetu ilikamata nafasi ya tatu,” anasema.
Anasema kushiriki kwake michezo hiyo kulianza kumfungulia njia na mwaka uliofuata (2014), aliitwa tena katika timu ya Kanda kabla ya msimu huu kuteuliwa tena kwenye Umisseta akiwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Geita.
Anasema michezo hapa nchini imekuwa na changamoto nyingi hali inayomsukuma kusoma kwa bidii huku akitamani siku moja awe mtaalamu wa michezo ili kusaidia wengine.
“Mfano katika shule yetu, hata kocha hatuna, kipindi cha michezo nahodha ambaye ni mwanafunzi mwenzetu ndiye anabeba jukumu la kocha,” anasema Loveness.





