Sehemu kubwa ya shughuli za Serikali ya Marekani zimefungwa leo baada ya
wabunge wa nchi hiyo kushindwa kuutatua mgogoro wa bajeti. Hali hiyo
imetokea kwa mara ya kwanza baada ya miaka 17
Malaki ya watumishi wa serikali wanarudishwa nyumbani bila ya malipo na
idara nyingi za serikali zimeambiwa zifunge milango. Sehemu kubwa ya
shughuli za serikali ya Marekani zimefungwa kwa sababu serikali hiyo
haina bajeti ya matumizi ya kawaida. Mgogoro huo maana yake ni kwamba
wafanya kazi wa serikali kuu hadi milioni moja watapewa likizo bila ya
malipo.
Baadhi ya huduma za umma kama vile miradi ya utafiti wa tiba
zinazoendeshwa na idara za serikali pia zitasimama. Marekani imefikia
hatua hiyo baada ya baraza la seneti linalodhibitiiwa na chama cha Rais
Obama cha Demokratik kulikataa pendekezo la wajumbe wa chama cha
Republican la kuusimamisha mpango wa huduma za afya wa Rais Obama.
Wabunge wa chama cha Republican wanaolidhibiti baraza la wawakilishi
walitaka mchakato wa nipe nikupe na chama cha Demokratik. Wabunge wa
Republican walikuwa tayari kuipitisha bajeti lakini kwa sharti la
kuusimamisha mpango wa afya wa Obama ambao umeanza kutekelezwa leo.
Mpango wa Rais Obama wa huduma za afya kwa Wamarekani unavurugwa na wabunge wa Republican
Juu ya kufungwa kwa shughuli za serikali Rais Barack Obama amesema. "Kwa bahati mbaya bunge halikuutimiza wajibu wake." Hata hivyo baadhi ya wizara zitaendelea kufanya kazi kama vile ya ulinzi. Rais Obama aliwatumia wanajeshi ujumbe wa video kwa kusema. "Kama amirijeshi wenu nimehakikisha kwamba mtaendelea kuwa na uwezo, zana na yote mnayoyahitaji ili kuutekeleza wajibu wenu kwa taifa. Vitisho kwa taifa letu bado havijabadilika na hivyo tunawataka muwe tayari kwa dharura yoyote"
Kila upande unaulaumu mwingine kwa kushindwa kufikiwa kwa makubaliano.
Rais obama ametahadhrisha juu ya madhara ya kiuchumi yanayoweza kutokea
kufuatia kusimamishwa kwa shughuli za serikali. Amesema kasi ya ustawi
wa uchumi inaweza kuvurugika.
Hatua iiyofikiwa leo pia inasababisha wasi wasi iwapo Marekani
italifikia lengo lake hadi kati kati ya mwezi wa oktoba la kuongeza deni
la serikali hadi dola Trilioni 16.7. Hisa barani barani Ulaya zimepanda
juu kidogo mapema leo lakini wawekaji vitega uchumi wameingiwa wasi
wasi.
Hata hivyo wachunguzi wanaamini kuwa wabunge wa Marekani watakaa chini
pamoja haraka ili kutafuta ufumbuzi. Licha ya kuwa suala muhimu kwa
masoko, madhali pana matumaini, masoko hayataathirika sana. Hayo
ameyasema mtaalamu wa masuala ya fedha wa Unicredit mjini Munic,
Christian Stocker. Wakati huo huo uchunguzi wa maoni umeonyesha kuwa
chama cha Republican kitalaumiwa na wananchi wengi wa Marekani kwa
kufungwa kwa shughuli za serikali.





